Nesi amchapa mjamzito ‘leba’, kitoto chafariki
Na Rachel Chibwete, Mwananchi
Kwa ufupi
Kwa sasa mama huyo, Mariamu Maroda yuko chumba cha
wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu (ICU) cha Hospitali ya Mkoa wa
Dodoma tangu Aprili 3, baada ya kufanyiwa upasuaji wa kukitoa kiumbe
hicho tumboni.
Dodoma. Muuguzi mmoja wa Kituo cha Afya cha
Muungano kilichoko wilayani Chamwino anatuhumiwa kumchapa viboko mma
mjamzito aliyekwenda kujifungua na kusababisha mtoto afie tumboni.
Kwa sasa mama huyo, Mariamu Maroda yuko chumba cha
wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu (ICU) cha Hospitali ya Mkoa wa
Dodoma tangu Aprili 3, baada ya kufanyiwa upasuaji wa kukitoa kiumbe
hicho tumboni.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, nduguwa mgonjwa huyo walimtuhumu
muuguzi huyo kuwa alifanya ukatili huo kwa kisingizio cha kutaka
kumlazimisha mama huyo asukume mtoto, akidai kuwa alikuwa anadeka.
Mama mdogo wa mama huyo, Joyce Charles alisema
kuwa muuguzi huyo alimchampa ndugu yao viboko katika sehemu mbalimbali
za mwili akiwa chumba cha uzazi kwa kile kilichoelezwa kushindwa
kujikakamua wakati wa kujifungua.
Charles alisema kuwa wakati wa uamuzi wa kumfanyia
upasuaji mama huyo kwenye Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, tayari mtoto
huyo alikuwa ameshafariki dunia kutokana na vipigo na muda mrefu
waliotumia tangu apelekwe kwenye kituo hicho hadi kuhamishiwa mjini.
“Tulitoka nyumbani Ijumaa usiku kumpeleka mtoto wa
dada yangu kwenye Zahanati ya Muungano kwa ajili ya kujifungua.
Tulipofika wodini wakati binti anasikia uchungu, nesi aliyekuwepo zamu
akaanza kumpiga kwenye mapaja na mgongoni akisema anadeka tu wakati
anaweza kujifungua,” alidai mama huyo mdogo wa Mariam.
“Wakati anapigwa nilikuwa naona, lakini sikuweza
kusema kitu kwa kuwa yeye ni nesi (hivyo nikahofia) asije akamuua.
Alimpiga na fimbo mpaka fimbo tatu zikakatika, alivyoona hali imekuwa
mbaya tukapewa ambulance (gari la wagonjwa) saa 12:00 asubuhi kutupeleka
hospitali ya misheni ya Mvumi na huko walivyoona hali ya mgonjwa
wakatupa chupa mbili za damu na Jumapili wakatuleta huku General
(Hospitali ya Mkoa wa Dodoma).”
Mama huyo alisema walivyofika hospitalini hapo
walimfanyia upasuaji wakamtoa mtoto, lakini bahati ikawa mbaya. Baada ya
operesheni wakampeleka wodini wakaona miguu inavimba na kupungua na
tumbo likaanza kujaa.
“Mtoto (Mariam) akaanza kulia anasema… mama
niombeeni…mama niombeeni. Dk Mzungu akafika akaniuliza huyu mtoto wako,
nikasema ndiyo, wakamtia sindano kwenye tumbo kuvuta ikatoka usaha
akasema huyu mtoto apelekwe chumba cha upasuaji.
“Wakati maelekezo yanatolewa, nikaulizwa, aende
nikasema mwache apelekwe nikaja kukaa mpaka saa 6:00 mchana. Wakamtoa
Mariam nikaambiwa niwape nguo na mpira wa kulia chakula akapelekwa ICU
na mpaka leo naona anaendelea vizuri angalau tofauti na walivyokuja,”
alisimulia.
Mdogo wa mgonjwa huyo, Silika Mkwawi mkazi wa
Kijiji cha Muungano alidai kuwa walimpeleka dada yake katika Zahanati
hiyo kwa ajili ya kujifungua saa 1:00 usiku. Baadaye daktari akasema
waende hospitali ya Mvumi bila kumchunguza kwa undani tatizo lake.
Muuguzi mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Anatoria Mkindo alikiri
kuwepo kwa mgonjwa huyo na kwamba kutokana na taarifa za tukio hilo,
wameagiza Ofisi ya Mganga Mkuu wa Chamwino kupeleka taarifa kwa RMO
kuhusu hatua zilizochukuliwa dhidi ya nesi aliyefanya kitendo hicho.
Naye Ofisa muuguzi anayemuhudumia katika chumba
cha ICU, Christina Mlumba alisema mgonjwa huyo alipelekwa baada ya
kufanyiwa operesheni na hali yake kwa sasa inaridhisha tofauti na
alivyofikishwa hapo.
Kaimu mganga mkuu wa mkoa wa Dodoma, Zainabu Chaula alisema kuwa
hakuwa na taarifa za mgonjwa huyo na kuomba muda ili aweze kufuatilia
na kutolea maelezo suala hilo.
Kamanda wa polisi Mkoa Dodoma, David Misime alisema hana taarifa ya tukio hilo na kuahidi kulifuatilia......