Miongoni mwa hazina muhimu kwa mwanadamu ni kuwa na uwezo wa kukumbuka
vitu kwa urahisi. Wanafunzi wengi hushindwa kufanya vizuri mitihani yao
kwa sababu ya kukabiliwa na tatizo la usahaulifu, ambao huchochewa na
mambo mengi ukiwemo ulevi wa pombe, utumiaji wa dawa za kulevya na
msongo wa mawazo ya kimaisha.
Licha ya uwezo wa kumbukumbu kupungua kutokana na umri wa mtu, sayansi
yaitegemei kijana mwenye umri wa chini ya miaka 28 kukabiliwa na tatizo
hili kwa kiwango kikubwa, ingawa wale wenye miaka zaidi ya 40 wanatajwa
kuzorota katika uwezo wa kukumbuka mambo.
Hata hivyo uchunguzi unaonesha kuwa watu ambao huzingatia suala la
kanuzi za afya zikiwemo mbinu za kukuza kumbukumbu ya akili hupunguza
kwa kiasi kikubwa mmeng�enyeko wa seli zinazojenga uwezo wa akili
katika kutunza kumbukumbu. (Susan Tapert mwanasaikolojia kutoka Chuo
cha California San Diego na kituo cha VA San Diego nchini Marekani
anathibitisha haya pia).
Hivyo basi, ili mwanafunzi aweze kuwa na uwezo wa kutunza vema mambo
anayosoma na kufundishwa na waalimu wake darasani lazima aweze
kuiongezea akili yake uwezo wa kutunza kumbukumbu kwa kufanya yafuatayo:
1 . LISHE BORA
Ni wazi kuwa wengi wetu tunafahamu maana ya lishe bora, lakini kwa
mujibu wa utafiti uliofanywa na Chuo cha American Academy of Neurology
kinachojihusisha na mambo ya neva, ulibaini kuwa machungwa, Spinachi,
Karoti, brokoli (aina fulani ya mboga kama kabichi), viazi vitamu na
mboga mboga huuongezea uhai ubongo na kumfanya mwanadamu asiweze
kushambuliwa na magonjwa wa kupooza.
Aidha matunda na vyakula vyenye vitamini B, Foliki Asidi (folic acid),
Niasini (niacin) Kalkumini (curcumin) husaidia kuufanya ubongo uwe na
mawasiliano ya kutosha na viungo vingine vya mwili na kupunguza kwa
asilimia 11 uhalibifu wa seli ndani ya ubongo. (Utafiti wa National
Research Council nchini Milan, Italy unathibitisha kuwa vyakula vyenye
Vitamini C na E hupunguza kiwango cha usahaulifu)
2. MAZOEZI YA MWILI
Ufanyaji wa mazoezi ya mwili huimarisha misuli na kusaidia akili kuweza
kufanya kazi vema, hii inatokana na ukweli kwamba tunapofanya mazoezi
tunakuwa tunaongeza msukumo wa damu mwilini na hivyo kuufanya ubongo
kufikiwa na damu ya kutosha ambayo ni muhimu kwa uimara wa kumbukumbu.
Mara nyingi, mazoezi yanayofaa zaidi kwa afya ya mwili na uimarisha wa
ubongo ni yale ya asubuhi na jioni. Kuhusu aina ya mazoezi inategemea na
umbo la mtu, lakini kukimbia, kuruka kamba, kucheza mpira na hata
kuinua vitu vizito vinavyolingana na uwezo wa mtu ni bora kwa afya.
Mazoezi ya aina hii yakifanywa na wanafunzi yanaweza kuwasaidia pia
kutunza kumbukumbu za masomo wanayofundishwa.
3 : MAZOEZI YA AKILI
Ni muhimu kwa mwanafunzi kuwa na mazoea ya kuifanyisha akili yake
mazoezi ya kutunza kumbukumbu kwa kuingiza kichwani mambo ambayo
hakuyazoea na kuyafanyia mazoezi ya kuyakumbuka. Kwa mfano mwanafunzi
anaweza kundika namba zisizopungua 14 na kuanza kuzitaja kwa kufuta
mpangilio aliojiwekea.
Namba zinatakiwa ziandikwe kwa kuchanganywa si kwa kuzifuatanisha kwa
mtindo wa kuhesabu. Mfano, 23938393835575, baada ya kuziandika kwa mfumo
huo mwanafunzi atatakiwa kuzikariri kwa dakika tano kisha kufumba macho
au kutazama pembeni na kuanza kuzisoma kwa kufuata mfululizo huo, huku
akihakikiwa na mtu mwingine. Mazoezi haya yatamsaidia kuondoa tatizo la
kusahau na kumpa kipimo ni kwa kiwango gani hana uwezo wa kukumbuka.
Endapo mwanafunzi atashindwa kufikia kiwango cha zaidi ya nusu ya namba
alizojiwekea afahamu kuwa ana uwezo mdogo wa kutunza kumbukumbu hivyo
anatakiwa kuongeza juhudi za kujiimarisha.
Njia nyingine ya kuifanyisha mazoezi akili ni kujifunza mara kwa mara
mambo mapya, ikiwa ni pamoja na kuimba nyimbo kwa lugha ya kigeni,
kujifunza lugha za makabila mengine, kutembelea mitandao mbalimbali ya
intaneti na kusoma, kucheza michezo ya kwenye simu na kompyuta.
Aidha usomaji wa vitabu, urudiaji wa mara kwa mara wa notisi za
darasani, husaidia kuongeza msukumo wa akili katika kutunza kumbukumbu
kichwani. Hata hivyo tafiti nyingi zinaonesha kuwa uhudhuriaji wa
majadala na uongeaji wa mambo ya msingi mbele ya watu wengi huimarisha
uwezo wa mtu kukumbuka mambo kwa urahisi.
4. UTUMIAJI WA VINYWAJI
Vinywaji kama kahawa, chai nyeusi navyo huchangia kuongeza uwezo wa
ubongo kutunza kumbukumbu. Inashauriwa kwa mwanadamu kutumia walau
kikombe kimoja cha vinywaji hivyo ili kuongeza enzymes ambazo ni muhimu
kwa kuuongezea nguvu ubongo ili uweze kutunza kumbukumbu. Hata hivyo
vinywaji vikali kama pombe haviruhusiwi kwani huchangia kudumaza uwezo
wa kukumbuka.
5. PUNGUZA MSONGO WA MAWAZO
Ubongo unaweza kushindwa kutunza kumbukumbu endapo mtu husika atakuwa na
msongo wa mawazo yatokanayo na shida za kidunia. Endapo mwanafunzi
atakuwa mtu mwenye kuutumikisha ubongo wake katika mawazo yenye kuumiza
kila wakati, hawezi kuwa na uwezo wa kukumbuka anayofundishwa.
Hivyo ni vema kupunguza mawazo kwa kuwashirikisha wengine magumu
unayokutana nayo maishani na kukubali kuyaacha yapite ili yakupe nafasi
ya kuishi kama wewe. Hatari ya msongo wa mawazo ni kuongeza kiwango cha
seli za cortisol ambayo huharibu ubongo wa kati ambao ni muhimu kwa
kutunza kumbukumbu.
6. KULALA
Watu wengi wakiwemo wanafunzi wamekuwa wakipuuza usingizi kwa kusoma
sana usiku na kuacha kupumzisha miili yao kwa kulala, jambo ambalo hili
ni hatari kwa utunzaji wa kumbukumbu kichwani.
Ifahamike kuwa usingizi ni kama chujio la akili ya mwanadamu, ambapo mtu
anapolala mchakato hufanyika akilini kwa kuyachambua mamilioni ya mambo
ambayo mhusika aliyaona, kuyasikia, kuhisi na pengine kuyatenda.
Mchakato huo huweza kuchuja mambo mabaya na kuyatupa na mema
huhifadhiwa kwenye kumbukumbu.
Hivyo, kama mwanafunzi hatolala, mambo yote yakiwemo ya kipuuzi
aliyofanya mchana yatabaki kwenye akili yake na kama mtindo huo wa
kutolala utaendelea unaweza kuufanya ubongo uchoke na kupoteza
kumbukumbu ya mambo muhimu yakiwemo ya shuleni.
Utafiti uliofanywa mwaka 2008 na Chuo cha Pennsylvania ulionesha kuwa
wanafunzi wanaolala kwa saa 6 kwa siku huwa na kumbukumbu nzuri zaidi ya
wale wanaolala kwa kiwango cha chini ya saa hizo. Utafiti wa aina hii
ulifanywa pia na Chuo Cha Luebeck na kubainisha kuwa akili huongezewa
uwezo mara tufu kwa kutunza kumbukumbu pale mtu anapokuwa analala
usingizi mnono.
7. TUMIA MUZIKI
Muziki unatajwa kuwa na faida katika kumsaidia mtu kukumbuka mambo
yaliyopita, inawezekana kabisa kwa kupita wimbo ukakumbuka mambo ambayo
uliyafanya siku za nyuma. Hivyo kuufurahisha mwili kwa kucheza muziki,
kusikiliza nyimbo, kunaweza kuongeza uwezo wa mtu kukumbuka mambo. Hata
hivyo kujifunza lugha au jambo fulani kwa njia ya wimbo ni rahisi
kukumbuka kuliko kuhifadhi maneno yenyewe.
8. KUANDIKA
Ni muhimu kwa mwanafunzi kuwa na kumbukumbu za pembeni nikiwa na maana
ya maandishi ya mkono. Ni muhimu kuorodhesha mambo ambayo umekusudia
kuyafanya au yalikutokea kwa kuyaandika kwenye kitabu kidogo cha
kumbukumbu. Mfano, unaweza kuandika siku uliyoanza shule, uliyozaliwa,
tarehe uliyomaliza darasa la saba n.k.
9. ONDOA HOFU
Kuna wanafunzi wengine hushindwa kukumbuka mambo si kwa sababu akili
imesahau, bali wanajichanganya kwa hofu na kutojiamini kwamba
wanachokumbushwa na akili kwa wakati huo kiko sahihi. Hivyo ni wajibu wa
mtu kujiamini na kutupilia mbali wasi wasi wote unaojitokeza wa kuhofu
kuchekwa au kutofanya vizuri katika jambo lililopo mbele yake.
10. AFYA
Jambo la mwisho ambalo ni muhimu katika uimarishaji kumbukumbu za
kichwani ni mtu kuwa na afya kwa maana ya kuhakikisha kuwa anatibiwa
magonjwa yake na anakuwa mfuasi mzuri wa huduma za kitabibu kwa ajili ya
kuuwesha mwili wake ufanye kazi kama unavyokusudia.
No comments:
Post a Comment