Sunday, April 26, 2015

NESI AMCHAPA MJAMZITO (LEBA) KITOTO CHAFARIKI

Nesi amchapa mjamzito ‘leba’, kitoto chafariki


Mhudumu katika kitengo cha watoto wachanga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Teddy Mganga akikihudumia kichanga chenye umri wa wiki baada ya kufikishwa na wasamaria wema hospitalini hapo waliomuokota kutoka katika kichaka, eneo la Shule ya msingi Mafiga B Manispaa ya Morogoro juzi. Picha na Juma Mtanda.      
Na Rachel Chibwete, Mwananchi
 
 
Kwa ufupi
Kwa sasa mama huyo, Mariamu Maroda yuko chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu (ICU) cha Hospitali ya Mkoa wa Dodoma tangu Aprili 3, baada ya kufanyiwa upasuaji wa kukitoa kiumbe hicho tumboni.


Dodoma. Muuguzi mmoja wa Kituo cha Afya cha Muungano kilichoko wilayani Chamwino anatuhumiwa kumchapa viboko mma mjamzito aliyekwenda kujifungua na kusababisha mtoto afie tumboni.
Kwa sasa mama huyo, Mariamu Maroda yuko chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu (ICU) cha Hospitali ya Mkoa wa Dodoma tangu Aprili 3, baada ya kufanyiwa upasuaji wa kukitoa kiumbe hicho tumboni.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, nduguwa mgonjwa huyo walimtuhumu muuguzi huyo kuwa alifanya ukatili huo kwa kisingizio cha kutaka kumlazimisha mama huyo asukume mtoto, akidai kuwa alikuwa anadeka.
Mama mdogo wa mama huyo, Joyce Charles alisema kuwa muuguzi huyo alimchampa ndugu yao viboko katika sehemu mbalimbali za mwili akiwa chumba cha uzazi kwa kile kilichoelezwa kushindwa kujikakamua wakati wa kujifungua.
Charles alisema kuwa wakati wa uamuzi wa kumfanyia upasuaji mama huyo kwenye Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, tayari mtoto huyo alikuwa ameshafariki dunia kutokana na vipigo na muda mrefu waliotumia tangu apelekwe kwenye kituo hicho hadi kuhamishiwa mjini.
“Tulitoka nyumbani Ijumaa usiku kumpeleka mtoto wa dada yangu kwenye Zahanati ya Muungano kwa ajili ya kujifungua. Tulipofika wodini wakati binti anasikia uchungu, nesi aliyekuwepo zamu akaanza kumpiga kwenye mapaja na mgongoni akisema anadeka tu wakati anaweza kujifungua,” alidai mama huyo mdogo wa Mariam.
“Wakati anapigwa nilikuwa naona, lakini sikuweza kusema kitu kwa kuwa yeye ni nesi (hivyo nikahofia) asije akamuua. Alimpiga na fimbo mpaka fimbo tatu zikakatika, alivyoona hali imekuwa mbaya tukapewa ambulance (gari la wagonjwa) saa 12:00 asubuhi kutupeleka hospitali ya misheni ya Mvumi na huko walivyoona hali ya mgonjwa wakatupa chupa mbili za damu na Jumapili wakatuleta huku General (Hospitali ya Mkoa wa Dodoma).”
Mama huyo alisema walivyofika hospitalini hapo walimfanyia upasuaji wakamtoa mtoto, lakini bahati ikawa mbaya. Baada ya operesheni wakampeleka wodini wakaona miguu inavimba na kupungua na tumbo likaanza kujaa.
“Mtoto (Mariam) akaanza kulia anasema… mama niombeeni…mama niombeeni. Dk Mzungu akafika akaniuliza huyu mtoto wako, nikasema ndiyo, wakamtia sindano kwenye tumbo kuvuta ikatoka usaha akasema huyu mtoto apelekwe chumba cha upasuaji.
“Wakati maelekezo yanatolewa, nikaulizwa, aende nikasema mwache apelekwe nikaja kukaa mpaka saa 6:00 mchana. Wakamtoa Mariam nikaambiwa niwape nguo na mpira wa kulia chakula akapelekwa ICU na mpaka leo naona anaendelea vizuri angalau tofauti na walivyokuja,” alisimulia.
Mdogo wa mgonjwa huyo, Silika Mkwawi mkazi wa Kijiji cha Muungano alidai kuwa walimpeleka dada yake katika Zahanati hiyo kwa ajili ya kujifungua saa 1:00 usiku. Baadaye daktari akasema waende hospitali ya Mvumi bila kumchunguza kwa undani tatizo lake. Muuguzi mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Anatoria Mkindo alikiri kuwepo kwa mgonjwa huyo na kwamba kutokana na taarifa za tukio hilo, wameagiza Ofisi ya Mganga Mkuu wa Chamwino kupeleka taarifa kwa RMO kuhusu hatua zilizochukuliwa dhidi ya nesi aliyefanya kitendo hicho.
Naye Ofisa muuguzi anayemuhudumia katika chumba cha ICU, Christina Mlumba alisema mgonjwa huyo alipelekwa baada ya kufanyiwa operesheni na hali yake kwa sasa inaridhisha tofauti na alivyofikishwa hapo.

Kaimu mganga mkuu wa mkoa wa Dodoma, Zainabu Chaula alisema kuwa hakuwa na taarifa za mgonjwa huyo na kuomba muda ili aweze kufuatilia na kutolea maelezo suala hilo.
Kamanda wa polisi Mkoa Dodoma, David Misime alisema hana taarifa ya tukio hilo na kuahidi kulifuatilia......

No comments:

Post a Comment