Tuesday, December 23, 2014

JINSI YA KUJIKOMBOA KIMAISHA KWA VIJANA

Jinsi ya Kujikomboa Kimaisha Kwa Vijana Hapa chini kuna muongozo wa kumfanya kijana afanikiwe kimaisha. UNACHOAMINI Njia ya kwanza ya kijana kujikomboa inaanzia kwenye kile anachoamini katika maisha yake. Katika hali ya kawaida mwanzo wa imani ya mwanadamu hutoka kwa wazazi wake na wakati mwingine mazingira atakayokulia. Kwa mfano, wengi tumekuwa na dini kwa sababu tulizaliwa na wenye dini, kwa maana hiyo hata tunachokiamini hatukuchagua kwa akili zetu wenyewe. Kwa msingi huo, kama kuna walio na dini mbaya (nataja tu), wengi wao wameponzwa na kile walichorithishwa na wazazi wao. Hali iko hivyo kwenye njia hii ya kwanza ya kijana kuelekea kwenye mafanikio. Wengi tumezaliwa na kurithishwa imani ya kutofanikiwa. Wazazi wetu walitulea kwa kutuambia maisha ni magumu, hatuwezi kufanikiwa, sisi ni masikini, duni na maneno kama hayo ya kukatisha tamaa. Hata hivyo, walifika mbali zaidi ya hapo kwa kutuita majina “mbwa, nyani, wajinga, wapumbavu, vichaa na waliolaaniwa. Ushahidi wa hili upo mpaka leo, kuna wazazi wanawaita watoto wao majina ya aina hiyo. Kwa hiyo, tukakua tukiamini kuwa sisi ni watu duni ambao hatuwezi kufanikiwa na kama tukiona mafanikio sehemu yoyote tunakuwa na mawazo kuwa, hiyo ni zawadi ya akina fulani wa ukoo mwingine, lakini siyo sisi. Mawazo ya vijana wengi leo yanaamini kuwa, umasikini ni mzigo mkubwa usiokuwa na ufumbuzi. Kitaalamu mtu anapokuwa na mawazo ya kutokufanikiwa hawezi kufanikiwa kwa sababu mafanikio huhitaji nguvu na nguvu za mwili haziwezi kujitokeza kama hazikuvutwa kufanya kazi. Kwa msingi huo, ili mtu aweze kufanikiwa lazima mawazo yake yakubali kuwa mafanikio ni sehemu ya lazima katika maisha. Jambo hili haliwezi kutokea mpaka kijana mwenyewe aliyelelewa kwenye mawazo ya kushindwa apigane vita na mawazo ya kutofanikiwa na kuyashinda. Njia pekee ya kujikomboa na mawazo mgando ni kufuta na kupuuza kauli zote alizoambiwa na wazazi wake kuhusu maisha magumu na kuanza kuamini kuwa, maendeleo ni yake na kwamba muda unahitajika kuyafikia. Nakushauri kijana mwenzangu kuanzia leo uyakatae mawazo ya kushindwa na kukubali udhaifu wako kwamba huwezi kufanikiwa kwa sababu yoyote ile, sema LAZIMA UFANIKIWE KWA KUWA UWEZO HUO UNAO. UNACHOTENDA Ukiangalia tabia ya maisha ya mwanadamu utagundua kuwa anafahamu mambo mengi sana, lakini hatendi sawa na ufahamu wake. Naamini hata vijana wanajua njia za kufanikiwa, lakini hawazifuati. Binafsi kuwafundisha watu kile wanachokifahamu ni sawa na ujinga. Kamwe siwezi kutumia muda wangu kuwaambia vijana ili waendelee wanahitaji kufanya biashara, kuajiriwa, kujiajiri kulima, kwani kufanya hivyo ni kukosa shabaha ya elimu. Ukitaka kuthibitisha hili zungumza na vijana wanaoishi maisha magumu uone kama hawatakuorodheshea njia zaidi ya 100 za kufanikiwa kimaisha! Kumbe tatizo lao si kujua bali ni kutenda ambako ndiyo njia ya kuelekea kwenye mafanikio. Wewe kama kijana jaribu kukumbuka ni biashara, mradi, kazi gani uliyokwishaiwaza na mpaka leo hujaanza kuifanya kwa sababu ambazo hazifahamiki? Miongoni mwa watu wenye tatizo hili wapo ambao si tu kwamba wana wazo, wana fedha, nguvu bali wana uwezo wa kufanya mambo yakawezekana, lakini wamejikuta hawafanyi yale wanayoyaweza na hivyo kubaki watumwa wa umasikini wakiamini tu kuwa, ipo siku wataanza na kufanikiwa. Tatizo kubwa katika mgando huu wa mawazo ni woga wa kushindwa na ugumu wa kuanzisha jambo. Wanasema waswahili ‘MWANZO MGUMU’ hata hivyo haiwi sababu ya wengi kushindwa kufanya mambo kwa kuhofia kukutana na ugumu. Watu wengi waliofanikiwa duniani ni wale ambao walikuwa tayari kuingia katika hatua hii muhimu ya kutenda yale waliyoyawaza na kuyathibitisha kuwa yatasukuma mbele maisha yao. Wote tunajua mwanzo wa kila kitu ni wazo, lakini mawazo yasiyokuwa na matendo ni upuuzi! Vitu ambavyo vimekuwepo duniani na vitakavyokuwepo baadaye vitatokana na ushirikiano wa hatua hizi mbili yaani KUAMINI NA KUTENDA. Ni wakati wako wa kuamini au kugeuza mawazo yako kuwa vitu halisi. Umewaza sana kujenga nyumba mbona hujaanza kujenga? Unasubiri nini kuanza biashara uliyoifanyia utafiti na ukagundua kuwa itakuingizia kipato. Nani kakuzuia usipange chumba chako na kuanza maisha yako? Amka na uanze kufanya yote uliyoyawaza! UNACHOCHAGUA Katika hali ya kawaida mwanadamu wa kawaida ana mahitaji mengi yanayotoka kwenye vitu vingi pia. Ukihitaji mchumba kwa mfano, itakulazimu hitaji lako likutane na wingi wa wachumba tofauti tofauti. Changamoto utakayokutana nayo wakati utakapokuwa unataka kutenda ulichoamini ni kuchagua. Tambua kuwa chochote utakachotaka duniani hakiko peke yake, ukienda sokoni kununua nyanya, utakutana na mafungu mengi ya bidhaa hiyo kiasi cha kukufanya utumie akili kuchagua fungu moja au mawili unayohitaji. Kuwepo na vitu vingi vya kuchagua kama nilivyosema ni moja kati ya tatizo kubwa linalowafanya vijana wengi washindwe kufanikiwa kimaisha kutokana na kutokuwa makini wakati wa kuchagua. Wapo ambao wameshindwa kuendelea kwa sababu tu walichagua wake wabaya, biashara, fani, kazi, kilimo kibaya na mambo mengine. Inawezekana kabisa pengine hata mambo ambayo yanakuendea kombo leo yametokana na kosa lako la kuchagua. Ushauri wangu ni kwamba kila mtu anayetaka kufanikiwa kimaisha lazima ahakikishe mambo anayoyachagua yawe ni yale aliyoyahakiki kuwa yanafaa. TUNACHOPATA Katika hali ya kawaida hakuna mtu anayetafuta kila siku asipate, hili halina ubishi, labda kinachoweza kuwa tofauti ni kiwango cha kupata.

Saturday, December 6, 2014

Tuesday, November 25, 2014

MBINU ZA MAFANIKIO KWA WAFANYABIASHARA

KATIKA haya mabadiliko ya milenia mpya, wajasiriamali wameweza kujitofautisha na wafanyabiashara wakubwa ili kuwaridhisha wateja wao. Kuwa na ujuzi, ustadi na uwezo wa kupigania kupata bidhaa bora ni njia mahususi ya kufanikisha biashara. Hivyo basi, mjasiriamali au mfanyabiashara mkubwa anatakiwa kuwa na mipango mizuri na ya kitafiti kufanikisha hili, kwani huo ni ufunguo wa mafanikio. Mara nyingi mfanyabiasgara lazima awe mbunifu. Hivyo unatakiwa kuwa mfikiriaji mzuri wa kuuza bidhaa unazozivumbua. Ni muhimu kuongeza thamani katika bidhaa ulizo nazo na huduma zako. Unapokuwa mjasiriamali unatakiwa kuwa na uvumbuzi wa mawazo yanayofanana na biashara yako kwa kuongeza thamani au huduma. Kwa matokeo hayo wateja watagundua ubora wakati watakapoona uhalisia wa bidhaa ulizo nazo. Unapotaka kuwa mfanyabiashara wa kiwango cha kuthaminiwa inakubidi uwe mtawala mzuri na meneja aliyebobea. Uwe hodari katika kujifunza na kupata faida ya teknolojia mpya ili iweze kukusaidia kukuza biashara yako katika uchumi mpya. Kukamilisha teknolojia mpya katika biashara yako ni lazima, hivyo utaendelea kukuza na kuifanya iende na wakati. Uwe mwendelezaji anayelenga kuimarisha mtandao. Kujihusisha na wafanyabiashara wengine ni muhimu sana kwa kuwa itakusaidia katika ukuaji wa biashara yako. Pia kuwa mwangalifu kuimarisha mawasiliano uliyo nayo kwa wateja wako na kujenga mawasiliano mengine mapya ili uweze kuwa na mazingira ya kiushindani. Baadhi ya mbinu za kufanya mabadiliko mazuri katika biashara yako ni pamoja na uwazi, mpango wa kibiashara ulio wazi au unaoeleweka na utaalamu. Uwazi unahitajika katika biashara yako, hivyo ni muhimu kutozuia habari zozote muhimu na kuwa mkweli kwa wateja wako. Kuwa na mpango wa biashara inayoeleweka kunakufanya uweze kuimarisha ubora wa bidhaa na huduma, ili kufikia mahitaji ya wateja wako na kuwaridhisha. Mpango wako wa biashara mara zote uwe unauangalia na kuuimarisha uweze kuelewa mabadiliko na mahitaji ya wateja wako. Unatakiwa kuimarisha na kutathmini utaalamu ulio nao ili kuweza kufanya kilicho bora zaidi. Usisahau kwamba unahitaji kutoa muda ili kuzingatia eneo lako la utaalamu ulionao. Kumbuka matangazo na masoko kwa biashara ndogo yanaongeza bidii na mipango ya kukuwezesha kufanikiwa zaidi. Wamiliki wengi wa biashara ndogo ndogo wanavunjwa moyo kwa haraka kwa sababu hawaelewi upepo wa biashara kwa wateja wao wanaowategemea baada ya kufanya kampeni ya matangazo yao ya awali. Matangazo ni sanaa inayokuwezesha kutazama na kutengeneza mpango wa muda mrefu utakaokuongoza katika mafanikio. Kuna mambo matatu wamiliki wa biashara ndogo ndogo wanayoweza kufanya katika kuongeza nafasi ya mafanikio katika kampeni ya kutangaza. Kwanza, unatakiwa kujiaminisha katika mpango wako wa muda mrefu. Kama hukufanya hivyo bilashaka unahitaji mpango mwingine. Jambo jingine ni kuwa unapokuwa na mipango ya kufungua biashara ni matangazo. Kujitangaza ni njia moja nzuri sana, lakini nayo inahitaji kuwe na hiyo mipango ya kujitangaza. Angalau unatakiwa kuwa na mpango wa kutangaza biashara zako kwa miezi sita, lakini ukweli ni kwamba inatakiwa ujitangaze kwa mwaka mzima. Hii itakusaidia kuimarisha mkataba wa muda mrefu na watangazaji, kwani kwa kufanya hivyo utakuwa unapunguza gharama za uangazaji. Hii inakusaidia kufikia ukomo uliojiwekea wa uchapaji na kutoa ujumbe mbalimbali unaotaka uwafikie wateja wako katika vipindi mbalimbali vya mwaka. Na jambo la tatu ni ongezeko la thamani - kama biashara ndogo unashindana na ushirika wa wateja wako. Unatakiwa kuwa tofauti. Zungumza kutokana na kile wateja wako wanachokihitaji na jinsi ya kuwapatia, lakini pia unaweza kuwa sehemu ya wateja. Inaweza kukuvunja moyo wakati unashindana na biashara ndogo na kubwa endapo hutapata matokeo mazuri ya biashara kutokana na ulivyojitangaza. Ili kuleta utofauti unayo nafasi kubwa ya kupata wateja wote ambao hawakufanyi ukatulia. Pata faida kwa kutoa huduma za bure – huduma za kawaida ambazo wafanyabiashara wadogo wanashindwa kufaidika nazo ni kutoa taarifa kwa vyombo vya habari. Kama una bidhaa mpya au huduma au kitu chochote kipya katika kiwanda chako ambacho unafikiri kuwa wateja wako wanatakiwa kujua, andika taarifa kwa vyombo vya habari. Pia unaweza kutoa taarifa hiyo kwenye magazeti binafsi.

SIRI YA UTAJIRI

Kwa nini watu wengine ni matajiri ? Watu wengi wanajiuliza, "Siri ya utajiri ni nini?" Jee ni mbinu gani zinaweza kumsaidia mtu kupata utajiri? Siri kubwa ya utajiri ni kujifunza elimu ya namna ya kutafuta mtaji, kuwekeza kwa busara kwa namna ambayo daima panakuwa na ziada na faida. Kwa bahati mbaya sana, elimu hii haifundishwi darasani ila wanayo wafanyabiashara wachache na kila anayefanikiwa kujifunza siri hii huwa tajiri na huendelea kuificha. Kwa bahati nzuri, katika utafiti wagu nimeweza kuigundua siri ya utajiri. Kwa kuwa ninapenda wasomaji wangu waweze kufanikiwa na wapate manufaa kwa kununua kitabu hiki nimeamua kuiweka siri hii wazi:- - Siri ya kwanza ya kuelekea ukwasi ni kubuni mradi unaojipa, yaani unaoweza kuitoa ziada na faida. - Siri ya pili ya kuelekea kwenye utajiri ni kujifunza na kujenga tabia ya kuweka akiba - Siri ya tatu ni kuwekeza fedha hizo za akiba katika vitega uchumi ambavyo vinazalisha faida endelevu. - Siri ya nne ni kujifunza namna ya kufanya biashara na kuanzisha biashara yako ili iwe indelevu. Kuna njia mbili za namna ya kupata utajiri zenye uhakika. Njia ya kwanza ni njia ndefu ambapo wataalamu na watafiti wa masuala ya fedha wameigundua njia hii ni rahisi kuifuata kwa sababu haihitaji uwe na kipato kikubwa, wanashauri kwamba ujenge tabia ya kuweka akiba, anza kuweka akiba ya T.shs 1,000 kila siku sawasawa na TShs 30,000 kwa mwezi, matokeo yake ni kwamba kama utaweka akiba yako kwa kipindi cha miaka 65 bila riba yoyote utakuwa na akiba TSshs 23,725,000 (Milioni Ishirini na Tatu Mia Saba Ishirini na Tano Elfu). Kama utawekeza fedha hiyo na kupata riba ya asilimia 10% kwa kila mwaka itazaa na kukuletea TShs 2,750,000,000 (Bilioni Mbili na Milioni Mia Saba Hamsini). Hesabu hii inaweza ikakutisha na usiamini macho yako lakini hiyo ni siri ya nguvu ya hesabu na riba kama alivyozielezea mwanafizikia Enstein kwamba katika dunia hii hakuna kitu chenye nguvu kama hesabu za riba. Pengine njia hii inaweza kuwa ni ndefu sana na ya kukatisha tamaa. Wengi wetu hatuwezi kusubiri muda mrefu. Hivyo tungependa kuwa na mafanikio ya kiuchumi kwa haraka. Lakini nasisitiza kama kipato chako ni kidogo anza leo kuweka akiba ya TShs 1,000 kwa siku. Dundulizo la akiba hii hukutiririshia utajiri bila wewe kukusudia kwani utaweza kukidhi hitajiko la ghafla kama kuugua safari ya dharura gharama za likizo na hata kutumia mbinu hii kama mpango wa elimu kwa watoto wako iwapo utawaanzishia hivi mara tu kila mmojawapo anapozaliwa au unaweza kuutumia kama upanga wa siku zijazo kwa mirathi ukianza hivyo leo kwa kupangilia namna hiyo kwa kila kusudio lako la baadaye. Hebu tuangalie njia ya pili. - Njia ya pili ya mkato ni kuongeza kiwango cha kuweka akiba kama wewe ni mtu mwenye shughuli za kuzalisha ziada. Kipato chako kinaweza kuwa kinaongezeka kila mara. Badala ya kuweka akiba ya TShs 1,000 kwa siku jiwekee malengo ya kuweka akiba ya TShs 10,000. Anza kwa kutenga asilimia 10% ya mapato yako hadi utakapofikia lengo la TShs 10,000 au zaidi kwa siku. Badala ya lengo lako kutimia kwa miaka sitini na tano (65) litatimia haraka zaidi. Kwa mfano ukiweka akiba ya TShs 10,000 kwa siku kwa muda wa miaka sita na miezi sita bila riba yoyote utapata TShs. 23,725,000. Ukiwekeza fedha hiyo na kupata riba ya asilimia 10% kwa miaka sita na miezi sita utapata TShs. 33,917,505.78. Kama fedha hiyo utaendelea kuweka akiba kwa riba hiyohiyo hadi kufikia muda wa miaka kumi utapata TShs. 63,112,201.43. Kwa kuwa kitu cha muhimu hapa ni kuweka akiba na kuwekeza akiba hiyo katika kitegauchumi chenye kutoa faida kubwa, utajiuliza jee uwekeze kwenye kitega uchumi chenye kutoa faida kiasi gani? Wataalamu wa mambo ya fedha wanashauri kuwa uwekeze fedha yako kwenye kitegauchumi chenye kutoa faida ya angalau asilimia 10% Kwa mfano unaweza kuwekeza kwenye Akaunti ya TAJIRIKA ya Standard Chatered Bank" inatoa riba ya asilimia kumi 10% pia unaweza kuwekeza kwa kununua hisa katika soko la hisa na mitaji. Kwa wastani wa watafiti wa masuala ya fedha viwango vya mapato yatokanayo na hisa kwa gawio pamoja na kukua kwa mtaji ni zaidi ya asilimia 11% ambayo ni makubwa kwa kiwango cha kawaida cha asilimia kumi (10%). Baada ya kueleza siri ya namna ya kupata utajiri nitazitaja njia zingine ambazo zinaweza kukuwezesha kuwa tajiri. 1. Unaweza kurithi mali na fedha kutoka kwa wazazi wako. Hii ni njia ya kubahatisha kwani watu matajiri siyo wengi na hivyo watoto wenye bahati kama hii ni wachache pia. 2. Unaweza kusomea ujuzi au utaalamu katika fani yenye malipo mazuri na kujiajiri mwenyewe. Kwa mfano, unaweza kusomea fani kama ya Uanasheria, Uhasibu na Udaktari au ufundi / sanaa na kadhalika. 3. Unaweza kuanzisha biashara yako na kuiendesha ili kupata ziada kubwa. 4. Unaweza kuendeleza vipaji vyako na kuwa mwanamichezo au msanii wa kulipwa. 5. Unaweza kutunga vitabu juu ya suala lolote unalolijua. Kwa mfano, kama wewe ni mtu uliyebobea katika masuala ya muziki unaweza kutunga kitabu kinachofundisha watu namna ya kuwa mwanamuziki. Watunzi wengi wa vitabu ni matajiri wakubwa. Hii ni kazi unayoweza kuifanya mara moja lakini ukavuna matunda yake kwa muda mrefu sana. 6. Unaweza kuwa mbunifu na kuanza kuuza mawazo yako au kutumia chombo ulichokibuni kukuingizia fedha. 7. Unaweza kucheza bahati nasibu na kushinda. Tatizo hapa soko na wateja wa aina hii ya huduma ni haba. Hiki ni kitu cha kubahatisha na nimekitaja makusudi ili kuwapa onyo wasomaji kwani watu wengi wanapenda sana kucheza michezo ya kubahatisha. Uwezekano wa kutajirika kwa njia hii ni mdogo sana. Hivyo, nawashauri wasomaji kuachana na njia hii ya kutafuta utajiri. Nawashauri wachague njia yoyote inayofaa na inawezekana kwa kufuatana na mazingira yanayomzunguka mtu husika. Mkulima au mfugaji anaweza kuzingatia fani hii na kutajirika sana. Kwa kweli hakuna mipaka, hasa hapa kwetu Tanzania kwa sababu ya wingi wa fursa za kuweza kujishughulisha na kuwa tajiri. Maelezo ya kina juu ya aina ya biashara au mbinu unaweza kuzitumia kutafuta na kupata faida utayapata katika sehemu ya pili ya kitabu hiki. Inawezekana kuwa tofauti kati ya mtu tajiri na mtu maskini inatokana na kile tulichojifunza kutoka kwa wazazi wetu. Wazazi maskini huwaambia watoto wao wajitahidi kusoma sana ili wapate maksi nzuri darasani na ili baadaye waweze kupata kazi nzuri. Wakati wazazi matajiri huwapa watoto wao elimu ya namna ya kutafuta fedha. Kwa kawaida tukiwa shuleni tunapewa ripoti ya masomo. Katika maisha tunatakiwa kuwa na ripoti yetu ya maisha nayo ni orodha ya mali tulizonazo ikiwa ni pamoja na elimu ya kuzaliwa na ya kusomea na fedha taslimu zile zilizo katika hifadhi mbalimbali. Kwa kufuata tafsiri ya Umoja wa mataifa mtu masikini ni yule ambaye kipato chake hakizidi TShs 1,000 kwa siku. Inawezekana kuwa mfumo wa kifedha wa mtu maskini ni mfumo ambao humfanya kutumia kipato chake chote kulipia matumizi huwa hana ziada wala uwezo wa kuweka akiba hana madeni na hana mali. Mfumo wa fedha wa mtu mwenye kipato cha kati ni mfumo ambao humfanya kuwa na mali kama magari, nyumba na kadhalika. Mara nyingi mali hizo huwa zinapatikana kwa mikopo na hutumia mshahara kulipia matumizi na madeni, hasa kama madeni ni makubwa, mtu mwenye kipato cha kati anapaswa kumuona mshauri wa maswala ya biashara. Hatua anazoweza kuchukua ili kujikwamua na tatizo la madeni anaweza kulazimika kuuza baadhi ya mali zake ambazo amezinunua kwa kutaka kuonyesha ufahari tu na ambazo hazina umuhimu. Kwa mfano kama mtu ana magari matatu ya kutembelea, anaweza kuuza magari mawili kubaki na gari limoja na fedha atakayoiokoa kuiwekeza au kutumia kama mataji na kuanzisha biashara ili kujiongezea kipato. Mfumo wa mtu tajiri ni mfumo ambao unamwezesha kuwa na biashara yake, kumiliki mali nyingi, kuwa na fedha nyingi katika akiba na awe ameziwekeza kwenye vitega uchumi vinavyolipa faida kubwa zaidi ya asiliamia kumi, kama vile nyumba za kupangisha na hisa. Mtu huyu hana wasiwasi na maisha. Anaweza kusafiri au kuugua lakini vitegauchumi vyake vinaendelea kumwingizia fedha. Siri kubwa ya matajiri ni uwezo wa kutumia fedha na kuziwekeza kupata faida kubwa. Hiki ni kitabu cha vitendo. Yote unayoyasoma humu inabidi uyafanyie kazi ili yakusaidie. Tofauti kati ya maskini na tajiri iko katika kuchukua hatua. Tajiri hujifunza mambo ya kumwendeleza na kuchukua hatua kwa kutekeleza kwa vitendo yale anayojifunza na anayoyaona yanaweza kumuinua kiuchumi. Maskini huwa anajifunza mambo na kuyaacha kichwani bila kuchukua hatua au kuyafanyia kazi aliyojifunza na hivyo fursa ya kupata utajiri inampita hivihivi.

Mbinu za kusoma na kuelewa

Tunapozungumzia uelewa wa wanafunzi darasani tunakuwa tumeingia katika msitu mpana zaidi wa majibu, lakini ukweli unabaki kuwa ndani ya darasa linalofundiswa na mwalimu mmoja hutokea wanafunzi wengine wakaelewa zaidi na wengine wasielewe kabisa. Kuna wanafunzi na baadhi ya wanasayansi wanaamini kuwa kuna binadamu huzaliwa na uwezo mkubwa wa kuelewa zaidi ya wenzao, huu ni ukweli lakini si wa kuamini sana kwani kipimo cha kuhakikisha kuwa huyu ameumbwa hivyo hakuna zaidi ya kuangali tu yale ambayo yanatendwa na huyo anayeitwa ana akili za ziada au za kuzaliwa. Lakini wakati huo huo kuangalia ayatendayo mtu au kuangalia uelewa wake darasani hakutoshi kumpa sifa za kuwa na sababu ya kuwazidi wenzake ambao wameamua tu kutokusoma, kutomsikiliza mwalimu, kutozingatia wanachoelekezwa au wameharibiwa na masumufu ya dunia yakiwemo masuala ya mapenzi. Kwa maana hiyo, hawa ambao hawaelewi kwa sababu wanasoma huku wanawaza mambo ya kimapenzi au wanafikiria kwenda muziki au kucheza, hawawezi kuwekwa kwenye kundi la watu ambao hawakuzaliwa na akili bali waliojiharibu kwa kukosa kuufahamu ukweli. Hivyo basi, kuna kila sababu kwa mwanafunzi kupuuza fikra za kizembe zinazomfanya ajione kuwa anazidiwa na wenzake darasani kwa sababu yeye hakuzaliwa na akili nyingi. Kila binadamu mwenye akili timamu kwa mujibu wa tafiti za watalaamu wa masuala ya ufahamu ana uwezo mkubwa mara 1000 kuliko ule anaoutumia. Hii ina maana kuwa kama kuna mwanafunzi anaongoza darasa lenye watu 100, uwezo huo wa kuongoza anaweza kusonga nao mpaka akafikia kwa watu 1,000 na akifika hapo anaongeza mara 1,000 tena na tena. Huu ni uwezo wa ajabu sana alionao mwanadamu. Lakini wengi kati yetu tumeshindwa kusonga mbele mara elfu toka tulipo kwa sababu tumeshindwa kutumia kipawa chetu na tumeamini uongo kuwa kuna waliopendelewa tangu wanaumbwa. Ben Carson mwandishi mashuhuri na daktari bingwa wa magonjwa ya akili ambaye awali alikuwa akiburuza mkia darasani aliambiwa na mama yake aitwaye Sanya Carson maneno haya: �you can do anything they can do, only you can do it better� (Nukuu inapatikana ndani ya kitabu kiitwacho THINK BIG cha Ben Carson ukurasa wa 7) kwa tafsiri isiyo rasimi Ben aliambiwa na mama yake kuwa �unaweza kufanya wayafanyayo, lakini wewe unaweza kufanya zaidi yao� Mwanamke huyu alidumu kumwambia mwanae kuwa ni bora zaidi ya wengine na kumtaka aongeze bidii kila siku ili afikie lengo. Ben aliaamini aliyokuwa akiambiwa na kwa makusudi aliamua kujibidisha na hatimaye kufikia kiwango cha kuwa msomi mwenye kuheshimika ulimwenguni. Kimsingi kuna watu wengi ambao walipuuza kauli za kujiona duni na kufanikiwa katika mambo waliyokusudia kuyafanya. Huu ni ushahidi kuwa hajaumbwa mwanadamu kuwa wa mwisho darasani bali matokeo ya kushindwa ni lazima yapewe kwanza sababu za uzembe na maumbile yawe ni ya mwisho kufikiriwa. Ufuatao ni muongozo wa kumuwezesha mwanafunzi kusoma na kuelewa vema. -Kumzingatia mwalimu Wanafunzi wengi wanashindwa kufikia uelewa wa juu kwenye masomo yao kwa sababu hawawi makini wanapofundishwa darasani na waalimu wao. Kitendo cha kuweka mawazo nusu darasani na nusu nje ni kujiwekea kizingiti cha kuelewa kinachofundishwa. Ni muhimu kwa mwanafunzi kama nilivyosema awali kwamba ampende mwalimu wake na aone furaha kumsikiliza anapofundisha. Itakuwa vigumu kwa mwanafunzi kuelewa anachofundishwa kama anayemfundisha anamchukia eti tu kwa sababu jana alimwadhibu au alimfokea. Ifahamike kuwa, msingi mkubwa kabisa wa mwanafunzi kuelewa somo lo lote ni kuelewa anachofundiswa moja kwa moja toka kwa mwalimu wake. Kitendo cha kutoka darasani bila kujua kilichofundishwa ni jambo la hatari kwa maendeleo ya mwanafunzi kimasomo. Inashauri kuwa mwanafunzi anapoingia darasani anatakiwa kuwa makini na kufuata anachoongea mwalimu wake neno kwa neno, huku akinoti anachoelewa na asichoelewa, ili kama ni msaada wa kueleweshwa aombe muda mfupi baada ya mwalimu kumaliza kufundisha. Kurudia notisi Mara baada ya mwanafunzi kufundishwa na kuelewa, anatakiwa akifika nyumbani siku hiyo hiyo arudia yale aliyosoma kwa kujikumbusha alichosema mwalimu wake. Hii itamsaidia zaidi kuifanya akili itunze kumbukumbu ya somo alilofundishwa na hivyo kumfanya mwanafunzi kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kujikumbusha au kukumbuka atakapokuwa akifanya mtihani. Haifai kwa mwanafunzi kurejea nyumbani na kufunika madaftari bila kujikumbusha au kurudia siku mbili baada ya kufundishwa, kufanya hivyo kunaweza kutoa nafasi kwa akili kuyatupa aliyofundishwa kutokana na wingi wa masomo au mambo aliyoelekezwa kwa siku mbili au wiki nzima. -Kufanya uchambuzi Ni wajibu wa mwanafunzi kufanya uchambuzi wa notisi zake za shule kwa kuandika mchanganuo wenye maneno machache ya msingi kwenye daftari jingine au karatasi. Kufanya hivi kutamsaidia kupunguza wingi wa maneno ya kuhifadhi akilini hasa kwa wanafunzi wa ngazi za chini ambao wengi wao hutumia mbinu za kukariri ambazo ni hatari kwa kusahau haraka. Kwa mfano, wanafunzi anapofundishwa kuhusu ubadhilifu wa pesa ndani ya Benki Kuu ya Tanzania ï kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje maarufu kama EPA na kupewa takwimu na mlolongo mzima ulivyokuwa, anachotakiwa kufanya yeye ni kunyambua mambo ya msingi ambayo yatamuongoza katika kujibu maswali, kama kuwajua wahusika, mwaka wa skendo, kiasi kilichoibwa na kilichorudiswa. Mambo hayo machache akiyafahamu yatamfanya awe na uwezo wa kulielezea jambo hilo kwa kina mbele za watu na kuonekana mwenye ufahamu wa kutosha, lakini pia atajihakikishia uwezo wa kukabili jaribio au mtihani wo wote utakaokuja na swali la EPA. -Kujipima uelewa Kumsikiliza mwalimu, kurudia notisi na kufanya uchambuzi kunaweza kusitoe picha sahihi juu ya uelewa wa mwanafuzni katika yale anayosoma pamoja na uwezo wake wa kukumbuka aliyojifunza. Mwanafunzi ili ajipime kama akili yake imenakiri vema anatakiwa kutenga siku ndani ya wiki kwa kujitungia mitihani kutoka kwenye daftari zake, kuifanya na kujisahihisha mwenyewe. Hii itampa mhusika ufahamu wa kujua ni eneo gani kaelewa zaidi ya jingine na hivyo kujituma zaidi sehemu ambayo hajaelewa kwa kuuliza tena kwa mwalimu au kwa wenzake ambao anadhani wana ufahamu mkubwa kuliko yeye. Ni vibaya kusoma bila kujipima uwezo. Itapendeza kama wanafunzi watakuwa wakifanya mitihani ya kujipima kwenye vikundi kila wiki. -Kukuza ufahamu Ziko njia nyingi za mwanafunzi kukuza ufahamu wake lakini muhimu zaidi ni kusoma vitabu, kusikiliza habari kupitia vyombo vya mbalimbali na kushiriki katika mijadala ya wazi yenye kujadili masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi. Mwanafunzi hawezi kukuza ufahamu kama hajui masuala ya jamii yake, siasa za ulimwengu na hali ya uchumi wa ndani na nje na hayo yote yanapatikana kwa kusoma. Jambo jingine la msingi ni kwa mwanafunzi kuepukana na aibu ya kujieleza mbele za watu. Njia pekee ya kuhifadhi kumbukumbu ya kile alichosoma na kuwa na tabia ya kuwaeleza wengine. Kwa mfano, kama mwanafunzi atakuwa amefungua mtandao wa inteneti na kusoma habari za kupanda kwa uchumi wa Marekani anatakiwa awaeleze wenzake alichojifunza, vivyo hivyo atakaposoma vitabu au kutazama filamu. Kujua jambo na kutokulitenda ni ujinga sawa na mtu ambaye hajui kabisa. Aibu ya kuzungumza mbele za watu haifai ni vema mwanafunzi akajiamini na kujizoeza kueleza anachokifahamu mbele za watu.

Njia 10 za kuimarisha kumbukumbu kichwani

Miongoni mwa hazina muhimu kwa mwanadamu ni kuwa na uwezo wa kukumbuka vitu kwa urahisi. Wanafunzi wengi hushindwa kufanya vizuri mitihani yao kwa sababu ya kukabiliwa na tatizo la usahaulifu, ambao huchochewa na mambo mengi ukiwemo ulevi wa pombe, utumiaji wa dawa za kulevya na msongo wa mawazo ya kimaisha. Licha ya uwezo wa kumbukumbu kupungua kutokana na umri wa mtu, sayansi yaitegemei kijana mwenye umri wa chini ya miaka 28 kukabiliwa na tatizo hili kwa kiwango kikubwa, ingawa wale wenye miaka zaidi ya 40 wanatajwa kuzorota katika uwezo wa kukumbuka mambo. Hata hivyo uchunguzi unaonesha kuwa watu ambao huzingatia suala la kanuzi za afya zikiwemo mbinu za kukuza kumbukumbu ya akili hupunguza kwa kiasi kikubwa mmeng�enyeko wa seli zinazojenga uwezo wa akili katika kutunza kumbukumbu. (Susan Tapert mwanasaikolojia kutoka Chuo cha California San Diego na kituo cha VA San Diego nchini Marekani anathibitisha haya pia). Hivyo basi, ili mwanafunzi aweze kuwa na uwezo wa kutunza vema mambo anayosoma na kufundishwa na waalimu wake darasani lazima aweze kuiongezea akili yake uwezo wa kutunza kumbukumbu kwa kufanya yafuatayo: 1 . LISHE BORA Ni wazi kuwa wengi wetu tunafahamu maana ya lishe bora, lakini kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Chuo cha American Academy of Neurology kinachojihusisha na mambo ya neva, ulibaini kuwa machungwa, Spinachi, Karoti, brokoli (aina fulani ya mboga kama kabichi), viazi vitamu na mboga mboga huuongezea uhai ubongo na kumfanya mwanadamu asiweze kushambuliwa na magonjwa wa kupooza. Aidha matunda na vyakula vyenye vitamini B, Foliki Asidi (folic acid), Niasini (niacin) Kalkumini (curcumin) husaidia kuufanya ubongo uwe na mawasiliano ya kutosha na viungo vingine vya mwili na kupunguza kwa asilimia 11 uhalibifu wa seli ndani ya ubongo. (Utafiti wa National Research Council nchini Milan, Italy unathibitisha kuwa vyakula vyenye Vitamini C na E hupunguza kiwango cha usahaulifu) 2. MAZOEZI YA MWILI Ufanyaji wa mazoezi ya mwili huimarisha misuli na kusaidia akili kuweza kufanya kazi vema, hii inatokana na ukweli kwamba tunapofanya mazoezi tunakuwa tunaongeza msukumo wa damu mwilini na hivyo kuufanya ubongo kufikiwa na damu ya kutosha ambayo ni muhimu kwa uimara wa kumbukumbu. Mara nyingi, mazoezi yanayofaa zaidi kwa afya ya mwili na uimarisha wa ubongo ni yale ya asubuhi na jioni. Kuhusu aina ya mazoezi inategemea na umbo la mtu, lakini kukimbia, kuruka kamba, kucheza mpira na hata kuinua vitu vizito vinavyolingana na uwezo wa mtu ni bora kwa afya. Mazoezi ya aina hii yakifanywa na wanafunzi yanaweza kuwasaidia pia kutunza kumbukumbu za masomo wanayofundishwa. 3 : MAZOEZI YA AKILI Ni muhimu kwa mwanafunzi kuwa na mazoea ya kuifanyisha akili yake mazoezi ya kutunza kumbukumbu kwa kuingiza kichwani mambo ambayo hakuyazoea na kuyafanyia mazoezi ya kuyakumbuka. Kwa mfano mwanafunzi anaweza kundika namba zisizopungua 14 na kuanza kuzitaja kwa kufuta mpangilio aliojiwekea. Namba zinatakiwa ziandikwe kwa kuchanganywa si kwa kuzifuatanisha kwa mtindo wa kuhesabu. Mfano, 23938393835575, baada ya kuziandika kwa mfumo huo mwanafunzi atatakiwa kuzikariri kwa dakika tano kisha kufumba macho au kutazama pembeni na kuanza kuzisoma kwa kufuata mfululizo huo, huku akihakikiwa na mtu mwingine. Mazoezi haya yatamsaidia kuondoa tatizo la kusahau na kumpa kipimo ni kwa kiwango gani hana uwezo wa kukumbuka. Endapo mwanafunzi atashindwa kufikia kiwango cha zaidi ya nusu ya namba alizojiwekea afahamu kuwa ana uwezo mdogo wa kutunza kumbukumbu hivyo anatakiwa kuongeza juhudi za kujiimarisha. Njia nyingine ya kuifanyisha mazoezi akili ni kujifunza mara kwa mara mambo mapya, ikiwa ni pamoja na kuimba nyimbo kwa lugha ya kigeni, kujifunza lugha za makabila mengine, kutembelea mitandao mbalimbali ya intaneti na kusoma, kucheza michezo ya kwenye simu na kompyuta. Aidha usomaji wa vitabu, urudiaji wa mara kwa mara wa notisi za darasani, husaidia kuongeza msukumo wa akili katika kutunza kumbukumbu kichwani. Hata hivyo tafiti nyingi zinaonesha kuwa uhudhuriaji wa majadala na uongeaji wa mambo ya msingi mbele ya watu wengi huimarisha uwezo wa mtu kukumbuka mambo kwa urahisi. 4. UTUMIAJI WA VINYWAJI Vinywaji kama kahawa, chai nyeusi navyo huchangia kuongeza uwezo wa ubongo kutunza kumbukumbu. Inashauriwa kwa mwanadamu kutumia walau kikombe kimoja cha vinywaji hivyo ili kuongeza enzymes ambazo ni muhimu kwa kuuongezea nguvu ubongo ili uweze kutunza kumbukumbu. Hata hivyo vinywaji vikali kama pombe haviruhusiwi kwani huchangia kudumaza uwezo wa kukumbuka. 5. PUNGUZA MSONGO WA MAWAZO Ubongo unaweza kushindwa kutunza kumbukumbu endapo mtu husika atakuwa na msongo wa mawazo yatokanayo na shida za kidunia. Endapo mwanafunzi atakuwa mtu mwenye kuutumikisha ubongo wake katika mawazo yenye kuumiza kila wakati, hawezi kuwa na uwezo wa kukumbuka anayofundishwa. Hivyo ni vema kupunguza mawazo kwa kuwashirikisha wengine magumu unayokutana nayo maishani na kukubali kuyaacha yapite ili yakupe nafasi ya kuishi kama wewe. Hatari ya msongo wa mawazo ni kuongeza kiwango cha seli za cortisol ambayo huharibu ubongo wa kati ambao ni muhimu kwa kutunza kumbukumbu. 6. KULALA Watu wengi wakiwemo wanafunzi wamekuwa wakipuuza usingizi kwa kusoma sana usiku na kuacha kupumzisha miili yao kwa kulala, jambo ambalo hili ni hatari kwa utunzaji wa kumbukumbu kichwani. Ifahamike kuwa usingizi ni kama chujio la akili ya mwanadamu, ambapo mtu anapolala mchakato hufanyika akilini kwa kuyachambua mamilioni ya mambo ambayo mhusika aliyaona, kuyasikia, kuhisi na pengine kuyatenda. Mchakato huo huweza kuchuja mambo mabaya na kuyatupa na mema huhifadhiwa kwenye kumbukumbu. Hivyo, kama mwanafunzi hatolala, mambo yote yakiwemo ya kipuuzi aliyofanya mchana yatabaki kwenye akili yake na kama mtindo huo wa kutolala utaendelea unaweza kuufanya ubongo uchoke na kupoteza kumbukumbu ya mambo muhimu yakiwemo ya shuleni. Utafiti uliofanywa mwaka 2008 na Chuo cha Pennsylvania ulionesha kuwa wanafunzi wanaolala kwa saa 6 kwa siku huwa na kumbukumbu nzuri zaidi ya wale wanaolala kwa kiwango cha chini ya saa hizo. Utafiti wa aina hii ulifanywa pia na Chuo Cha Luebeck na kubainisha kuwa akili huongezewa uwezo mara tufu kwa kutunza kumbukumbu pale mtu anapokuwa analala usingizi mnono. 7. TUMIA MUZIKI Muziki unatajwa kuwa na faida katika kumsaidia mtu kukumbuka mambo yaliyopita, inawezekana kabisa kwa kupita wimbo ukakumbuka mambo ambayo uliyafanya siku za nyuma. Hivyo kuufurahisha mwili kwa kucheza muziki, kusikiliza nyimbo, kunaweza kuongeza uwezo wa mtu kukumbuka mambo. Hata hivyo kujifunza lugha au jambo fulani kwa njia ya wimbo ni rahisi kukumbuka kuliko kuhifadhi maneno yenyewe. 8. KUANDIKA Ni muhimu kwa mwanafunzi kuwa na kumbukumbu za pembeni nikiwa na maana ya maandishi ya mkono. Ni muhimu kuorodhesha mambo ambayo umekusudia kuyafanya au yalikutokea kwa kuyaandika kwenye kitabu kidogo cha kumbukumbu. Mfano, unaweza kuandika siku uliyoanza shule, uliyozaliwa, tarehe uliyomaliza darasa la saba n.k. 9. ONDOA HOFU Kuna wanafunzi wengine hushindwa kukumbuka mambo si kwa sababu akili imesahau, bali wanajichanganya kwa hofu na kutojiamini kwamba wanachokumbushwa na akili kwa wakati huo kiko sahihi. Hivyo ni wajibu wa mtu kujiamini na kutupilia mbali wasi wasi wote unaojitokeza wa kuhofu kuchekwa au kutofanya vizuri katika jambo lililopo mbele yake. 10. AFYA Jambo la mwisho ambalo ni muhimu katika uimarishaji kumbukumbu za kichwani ni mtu kuwa na afya kwa maana ya kuhakikisha kuwa anatibiwa magonjwa yake na anakuwa mfuasi mzuri wa huduma za kitabibu kwa ajili ya kuuwesha mwili wake ufanye kazi kama unavyokusudia.