Tuesday, November 25, 2014
Mbinu za kusoma na kuelewa
Tunapozungumzia uelewa wa wanafunzi darasani tunakuwa tumeingia katika
msitu mpana zaidi wa majibu, lakini ukweli unabaki kuwa ndani ya darasa
linalofundiswa na mwalimu mmoja hutokea wanafunzi wengine wakaelewa
zaidi na wengine wasielewe kabisa.
Kuna wanafunzi na baadhi ya wanasayansi wanaamini kuwa kuna binadamu
huzaliwa na uwezo mkubwa wa kuelewa zaidi ya wenzao, huu ni ukweli
lakini si wa kuamini sana kwani kipimo cha kuhakikisha kuwa huyu
ameumbwa hivyo hakuna zaidi ya kuangali tu yale ambayo yanatendwa na
huyo anayeitwa ana akili za ziada au za kuzaliwa.
Lakini wakati huo huo kuangalia ayatendayo mtu au kuangalia uelewa wake
darasani hakutoshi kumpa sifa za kuwa na sababu ya kuwazidi wenzake
ambao wameamua tu kutokusoma, kutomsikiliza mwalimu, kutozingatia
wanachoelekezwa au wameharibiwa na masumufu ya dunia yakiwemo masuala ya
mapenzi.
Kwa maana hiyo, hawa ambao hawaelewi kwa sababu wanasoma huku wanawaza
mambo ya kimapenzi au wanafikiria kwenda muziki au kucheza, hawawezi
kuwekwa kwenye kundi la watu ambao hawakuzaliwa na akili bali
waliojiharibu kwa kukosa kuufahamu ukweli.
Hivyo basi, kuna kila sababu kwa mwanafunzi kupuuza fikra za kizembe
zinazomfanya ajione kuwa anazidiwa na wenzake darasani kwa sababu yeye
hakuzaliwa na akili nyingi. Kila binadamu mwenye akili timamu kwa mujibu
wa tafiti za watalaamu wa masuala ya ufahamu ana uwezo mkubwa mara 1000
kuliko ule anaoutumia.
Hii ina maana kuwa kama kuna mwanafunzi anaongoza darasa lenye watu 100,
uwezo huo wa kuongoza anaweza kusonga nao mpaka akafikia kwa watu 1,000
na akifika hapo anaongeza mara 1,000 tena na tena. Huu ni uwezo wa
ajabu sana alionao mwanadamu. Lakini wengi kati yetu tumeshindwa kusonga
mbele mara elfu toka tulipo kwa sababu tumeshindwa kutumia kipawa chetu
na tumeamini uongo kuwa kuna waliopendelewa tangu wanaumbwa.
Ben Carson mwandishi mashuhuri na daktari bingwa wa magonjwa ya akili
ambaye awali alikuwa akiburuza mkia darasani aliambiwa na mama yake
aitwaye Sanya Carson maneno haya: �you can do anything they can do,
only you can do it better� (Nukuu inapatikana ndani ya kitabu
kiitwacho THINK BIG cha Ben Carson ukurasa wa 7) kwa tafsiri isiyo
rasimi Ben aliambiwa na mama yake kuwa �unaweza kufanya wayafanyayo,
lakini wewe unaweza kufanya zaidi yao�
Mwanamke huyu alidumu kumwambia mwanae kuwa ni bora zaidi ya wengine na
kumtaka aongeze bidii kila siku ili afikie lengo. Ben aliaamini
aliyokuwa akiambiwa na kwa makusudi aliamua kujibidisha na hatimaye
kufikia kiwango cha kuwa msomi mwenye kuheshimika ulimwenguni.
Kimsingi kuna watu wengi ambao walipuuza kauli za kujiona duni na
kufanikiwa katika mambo waliyokusudia kuyafanya. Huu ni ushahidi kuwa
hajaumbwa mwanadamu kuwa wa mwisho darasani bali matokeo ya kushindwa ni
lazima yapewe kwanza sababu za uzembe na maumbile yawe ni ya mwisho
kufikiriwa. Ufuatao ni muongozo wa kumuwezesha mwanafunzi kusoma na
kuelewa vema.
-Kumzingatia mwalimu
Wanafunzi wengi wanashindwa kufikia uelewa wa juu kwenye masomo yao kwa
sababu hawawi makini wanapofundishwa darasani na waalimu wao. Kitendo
cha kuweka mawazo nusu darasani na nusu nje ni kujiwekea kizingiti cha
kuelewa kinachofundishwa.
Ni muhimu kwa mwanafunzi kama nilivyosema awali kwamba ampende mwalimu
wake na aone furaha kumsikiliza anapofundisha. Itakuwa vigumu kwa
mwanafunzi kuelewa anachofundishwa kama anayemfundisha anamchukia eti tu
kwa sababu jana alimwadhibu au alimfokea.
Ifahamike kuwa, msingi mkubwa kabisa wa mwanafunzi kuelewa somo lo lote
ni kuelewa anachofundiswa moja kwa moja toka kwa mwalimu wake. Kitendo
cha kutoka darasani bila kujua kilichofundishwa ni jambo la hatari kwa
maendeleo ya mwanafunzi kimasomo.
Inashauri kuwa mwanafunzi anapoingia darasani anatakiwa kuwa makini na
kufuata anachoongea mwalimu wake neno kwa neno, huku akinoti anachoelewa
na asichoelewa, ili kama ni msaada wa kueleweshwa aombe muda mfupi
baada ya mwalimu kumaliza kufundisha.
Kurudia notisi
Mara baada ya mwanafunzi kufundishwa na kuelewa, anatakiwa akifika
nyumbani siku hiyo hiyo arudia yale aliyosoma kwa kujikumbusha
alichosema mwalimu wake. Hii itamsaidia zaidi kuifanya akili itunze
kumbukumbu ya somo alilofundishwa na hivyo kumfanya mwanafunzi kuwa
katika nafasi nzuri zaidi ya kujikumbusha au kukumbuka atakapokuwa
akifanya mtihani.
Haifai kwa mwanafunzi kurejea nyumbani na kufunika madaftari bila
kujikumbusha au kurudia siku mbili baada ya kufundishwa, kufanya hivyo
kunaweza kutoa nafasi kwa akili kuyatupa aliyofundishwa kutokana na
wingi wa masomo au mambo aliyoelekezwa kwa siku mbili au wiki nzima.
-Kufanya uchambuzi
Ni wajibu wa mwanafunzi kufanya uchambuzi wa notisi zake za shule kwa
kuandika mchanganuo wenye maneno machache ya msingi kwenye daftari
jingine au karatasi. Kufanya hivi kutamsaidia kupunguza wingi wa maneno
ya kuhifadhi akilini hasa kwa wanafunzi wa ngazi za chini ambao wengi
wao hutumia mbinu za kukariri ambazo ni hatari kwa kusahau haraka.
Kwa mfano, wanafunzi anapofundishwa kuhusu ubadhilifu wa pesa ndani ya
Benki Kuu ya Tanzania ï kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje maarufu
kama EPA na kupewa takwimu na mlolongo mzima ulivyokuwa, anachotakiwa
kufanya yeye ni kunyambua mambo ya msingi ambayo yatamuongoza katika
kujibu maswali, kama kuwajua wahusika, mwaka wa skendo, kiasi
kilichoibwa na kilichorudiswa.
Mambo hayo machache akiyafahamu yatamfanya awe na uwezo wa kulielezea
jambo hilo kwa kina mbele za watu na kuonekana mwenye ufahamu wa
kutosha, lakini pia atajihakikishia uwezo wa kukabili jaribio au mtihani
wo wote utakaokuja na swali la EPA.
-Kujipima uelewa
Kumsikiliza mwalimu, kurudia notisi na kufanya uchambuzi kunaweza
kusitoe picha sahihi juu ya uelewa wa mwanafuzni katika yale anayosoma
pamoja na uwezo wake wa kukumbuka aliyojifunza. Mwanafunzi ili ajipime
kama akili yake imenakiri vema anatakiwa kutenga siku ndani ya wiki kwa
kujitungia mitihani kutoka kwenye daftari zake, kuifanya na
kujisahihisha mwenyewe.
Hii itampa mhusika ufahamu wa kujua ni eneo gani kaelewa zaidi ya
jingine na hivyo kujituma zaidi sehemu ambayo hajaelewa kwa kuuliza tena
kwa mwalimu au kwa wenzake ambao anadhani wana ufahamu mkubwa kuliko
yeye. Ni vibaya kusoma bila kujipima uwezo. Itapendeza kama wanafunzi
watakuwa wakifanya mitihani ya kujipima kwenye vikundi kila wiki.
-Kukuza ufahamu
Ziko njia nyingi za mwanafunzi kukuza ufahamu wake lakini muhimu zaidi
ni kusoma vitabu, kusikiliza habari kupitia vyombo vya mbalimbali na
kushiriki katika mijadala ya wazi yenye kujadili masuala ya kijamii,
kisiasa na kiuchumi.
Mwanafunzi hawezi kukuza ufahamu kama hajui masuala ya jamii yake, siasa
za ulimwengu na hali ya uchumi wa ndani na nje na hayo yote
yanapatikana kwa kusoma. Jambo jingine la msingi ni kwa mwanafunzi
kuepukana na aibu ya kujieleza mbele za watu. Njia pekee ya kuhifadhi
kumbukumbu ya kile alichosoma na kuwa na tabia ya kuwaeleza wengine.
Kwa mfano, kama mwanafunzi atakuwa amefungua mtandao wa inteneti na
kusoma habari za kupanda kwa uchumi wa Marekani anatakiwa awaeleze
wenzake alichojifunza, vivyo hivyo atakaposoma vitabu au kutazama
filamu. Kujua jambo na kutokulitenda ni ujinga sawa na mtu ambaye hajui
kabisa. Aibu ya kuzungumza mbele za watu haifai ni vema mwanafunzi
akajiamini na kujizoeza kueleza anachokifahamu mbele za watu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment