Dar es Salaam. Wadau wa elimu nchini wamekosoa
ufaulu wa matokeo ya darasa la saba yaliyotangazwa juzi kwa kusema siyo
ishara ya kukua kwa sekta hiyo, ilhali kuna tatizo la kisera.
Kauli hizo zimejitokeza baada ya Baraza la
Mitihani Tanzania (Necta), kutangaza ufaulu wa wanafunzi 451,392 kati ya
808,085 waliosajiliwa kufanya mtihani.
Katika ufaulu huo, somo la Kiswahili linaongoza
kwa asilimia 69.70, huku Kiingereza kikiwa ni asilimia 38.84,
ikilinganishwa na asilimia 35.52 za mwaka jana.
Katibu mtendaji wa Jumuiya ya Wamiliki wa Shule na
Vyuo Binafsi nchini (TAMONGSCO), Benjamin Nkonya alisema matokeo hayo
ni maandalizi ya wanafunzi kuanguka kimasomo katika ngazi ya sekondari
kwa kuwa watafundishwa kwa Kiingereza, lugha ambayo wengi hawaijui.
“Somo walilofeli ni Kiingereza, ambalo ndiyo
msingi wa kufaulu kwa ngazi ya sekondari. Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa
(BRN) unaweza kuwa mbwembwe tu, kwani tatizo hilo limekuwa la kisera,”
alisema na kuongeza:
“Hata mipango ya awali ya Upe (Elimu ya Msingi kwa
Wote) na MMEM (Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi) haikuonyesha
mafanikio yoyote, matokeo yake wanafunzi wanaotoka daraja hilo wanaishia
kupata alama ‘0’ kwa kudhani ni wajinga kumbe hawakuwa na uelewa wa
lugha ya kufundishia.”
Profesa George Shumbusho wa Chuo Kikuu cha Mzumbe
alisema pamoja na udhaifu wa matumizi ya lugha, kiwango hicho cha ufaulu
siyo ishara ya mafanikio.
Profesa Shumbusho alihoji inakuwaje wanaofaulu baadhi yao huwa hawafikii vigezo vya kuingia ngazi ya elimu ya sekondari.
“Wamefaulu nusu, lakini utakuta wengi wanaingia
kidato cha kwanza hawajui kusoma na kuandika, hawana uwezo na ufahamu wa
kutosha katika masomo? bado inatia shaka sana na wingi huo wa ufaulu,”
alisema.
“Mbali na hilo, hata wale wanaoshindwa kuendelea
na kidato cha kwanza wamejengewa uwezo gani katika masomo ya stadi za
kazi ili kujitegemea kwa kazi za kujiajiri?”
Mhadhiri mwandamizi wa Idara ya Saikolojia na
Mtalaa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Eugenia Kafanambo alisema
siyo sahihi kuhukumu matokeo hayo kwa sasa, kabla ya kuona uwezo wa
wanafunzi hapo baadaye.
Eugenia alisema mpango wa BRN unaweza kuwa sababu ya ufaulu huo kutokana na walimu kujizatiti katika utekelezaji wake.
No comments:
Post a Comment